Kupunguka kwa mvua kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya anga kumesababishia jiji la Cape Town tatizo kubwa la maji. Wakazi wa jiji hilo waliishi bila kufahamu ujio wa karibu wa siku ya Day Zero, iliyotabiriwa awali kwamba ingewadia mnamo Mei 13, 2018, siku ambayo maji yangeisha kwenye mifereji. Hatua za dharura za migao ya maji zilichukuliwa, na ikawabidi watu kupunguza matumizi ya maji kwa kiasi kikubwa, hadi kufikia kikomo cha galoni 13 za maji kwa mtu mmoja kwa siku. Jiji la Cape Town liliweza kuchelewesha ujio wa siku wa siku ya Day Zero kwa kuweka masharti makali huku likiathirika kiuchumi.

water-day-zero-limit-water

Udhibiti wa matumizi ya maji kwa wakazi wa Cape Town

Tatizo hili halishuhudiwi jijini Cape Town tu. Hata nchi ya Brazil yenye hifadhi kubwa zaidi ya maji yasiyo na chumvi duniani, ambayo ina asilimia 12 ya hifadhi ya dunia ya maji yasiyo na chumvi, pia inapitia Tatizo la Maji la pili la nchi hiyo katika miaka 5 iliyopita. Tatizo hilo ni sawa na lile la Cape Town, ambalo husababishwa na ongezeko la mahitaji ya maji huku mvua ikipungua kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya anga. Katika mwaka wa 2015, jiji la São Paulo, ambalo ni mojawapo ya majiji 10 yenye watu wengi zaidi duniani, lilishuhudia hifadhi yalo kuu ya maji ikiwa na chini ya asilimia 4 ya ujazo wayo.

Huku matini hii ikiandikwa, jiji lingine nchini Brazil tayari linapitia tatizo jipya la maji. Jiji la Curitiba, lenye takriban wakazi milioni 3.5, linashuhudia ukame mkali zaidi katika miaka 50 iliyopita. Jiji hilo linaweka mikakati ya mgao wa maji: maji yatasambazwa kwa saa 36 kisha usambazaji usitishwe kwa saa 36, na huenda kusitishwa huko kwa usambazaji kukaongezwa hadi saa 48 ikiwa mvua haitanyesha karibuni.

Tatizo la Maji la Dunia

Visa hivi ni mifano tu ya hali ambayo huenda ikazorota katika miaka ijayo. Takriban nusu ya watu wote ulimwenguni wanaishi katika maeneo yenye uwezekano wa kushuhudia uhaba wa maji kwa angalau mwezi mmoja kila mwaka (Burek na waandishi wengine, 2016). Maendeleo yanayofanyika kando mwa miji mikubwa yamechochea ongezeko la matatizo ya maji, na kusababisha mikakati ya usimamizi wa rasilimali maji kutekelezwa haraka ili kuhakikisha maji yanatunzwa kwa ajili ya miaka ijayo.

Idadi ya watu ulimwenguni itaongezeka kutoka bilioni 7.6 hadi kati ya bilioni 9.4 na bilioni 10.2 kufikia mwaka wa 2050, hivyo basi pia kuongeza matumizi ya maji. Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa, matumizi ya maji Ulimwenguni yameongezeka mara sita katika muda wa miaka 100 iliyopita, na yataendelea kuongezeka kwa kasi sawa ya takriban asilimia 1 kila mwaka kwa sababu ya kuongezeka kwa idadi ya watu, maendeleo ya kiuchumi na mitindo inayobadilika ya matumizi ya maji.

water-day-zero-water-supply

Mahitaji makubwa ya maji katika vyanzo vya maji vya umma

Ongezeko la matumizi ya maji pekee ni sababu tosha ya kututahadharisha kuhusu umuhimu wa kuhakikisha tunatunza maji. Hata hivyo, kuna hali nyingine tata: mabadiliko ya hali ya anga. Mitindo ya mifumo ya kihaidrolojia mara nyingi hubadilika wakati halijoto inaongezeka. Athari za mitindo ya mvua inayobadilikabadilika tayari zinashuhudiwa na utabiri unaonyesha kwamba katika miaka ijayo, vipindi vya ukame mkali vitatokea mara nyingi. Zaidi ya watu bilioni 5 huenda wakakumbwa na uhaba wa maji kufikia mwaka wa 2050 kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya anga (Umoja wa Mataifa, 2019).

Mahitaji ya maji yatazidi kiasi kilichopo kwa ajili ya matumizi kwa asilimia 40 kufikia mwaka wa 2030, kulingana na utabiri wa Umoja wa Mataifa, tukizingatia athari za mabadiliko ya hali ya anga, ongezeko la idadi ya watu, na shughuli za binadamu.

Huenda jiji la São Paulo liishiwe na maji tena katika miaka michache ijayo, lakini sio jiji hili tu. Tatizo la maji huenda likakumba miji mikubwa kama Bangalore, Beijing, Cairo, Jakarta, Moscow, Istanbul, Mexico City, London, Tokyo, na Miami.

Tutawezaje kupambana na tatizo la maji?

Kuna namna mbili za kusuluhisha tatizo la uhaba wa maji: kudhibiti tatizo lililopo au kuzuia kuibuka kwa matatizo mapya ya maji.

Wakati kuna tatizo la maji linaloendelea, sharti hatua za dharura zichukuliwe ili kupunguza matumizi kwa kutekeleza mgao wa maji. Biashara huenda zikafungwa. Jiji la Cape Town lilipiga marufuku biashara za kuosha magari, jambo lililosababisha ukosefu wa ajira. Duru za uzalishaji katika sekta za kilimo na viwanda pia zimo hatarini ya kupungua kwa uzalishaji kwa sababu ya uhaba wa maji. Tatizo la maji huenda likasababisha matatizo ya kiuchumi, migogoro inayoletwa na uhaba wa maji, na hatari kwa afya ya binadamu.

Iliwabidi wakazi wa Cape Town kuchagua kati ya kuoga na kusafisha nyumba. Hata hivyo, kwa kuwa tatizo la maji tayari lilikuwa limeanza, hatua zinazochukuliwa ni za kudhibiti matumizi ya maji tu ili kuhifadhi maji yaliyobaki.

Matokeo ya utabiri sio mazuri, ingawa tayari kuna teknolojia nyingi zinazoweza kusaidia kuzuia kutokea kwa siku zingine za Day Zero kote ulimwenguni na kuhakikisha kuna maji ya kutosha.

Tazama video hii ili ujifahamishe zaidi kuhusu maana ya siku ya Day Zero ▶️.

Kulingana na tabiri za Umoja wa Mataifa, kufikia mwaka wa 2030, mahitaji ya maji yatazidi ugavi wake kwa asilimia 40 kwa sababu ya jumla ya athari za mabadiliko ya hali ya anga, ongezeko la idadi ya watu, na mitindo ya binadamu

Elisa StefanMhandisi wa Mazingira na Mtafiti. Mtaalamu wa Usimamizi wa Rasilimali Maji

Hivi sasa tunaweza kuzuia matatizo mapya ya maji kwa kuchukua hatua za kimfumo zinazotuwezesha kuhifadhi maji, kwa kuboresha mifumo ya maji taka na kupunguza umwagikaji wa maji kwenye mifumo ya kusambaza maji, pamoja na hatua za kusasisha mifumo ya kutupa maji kwa kuboresha miundo msingi ya asili ya usimamizi wa maji ya mvua, na kuboresha uangalizi wa mifumo ya maji.

Watu pia wanaweza kupunguza matumizi ya maji nyumbani, kuchagua kutumia bidhaa zilizotengenezwa kwa maji ya kiwango kidogo, kuweka mifumo ya kunasa maji ya mvua, na kutumia maji yaliyokuwa yametumika tena. Wanaotumia maji katika sekta za viwanda na kilimo wanaweza kupunguza matumizi ya maji kwa kiasi kikubwa kwa kutekeleza teknolojia za kutumia tena maji yaliyokuwa yametumika tena na kuzuia umwagikaji wa maji wakati wa kutengeneza bidhaa, lakini wanahitaji kuanza kutekeleza hatua hizo sasa hivi.

Usimamizi wa rasilimali maji unahitaji kutekelezwa kwa ushirikiano miongoni mwa watumiaji wa maji na waamuzi ili kuhakikisha kutakuwa na maji ya kutosha katika siku zijazo. Ili kuepuka siku za Day Zero, itakuwa muhimu sana kutumia teknolojia mbalimbali zinazoweza kutambua data zinazohusiana na maji na kutambua mikakati bora zaidi ili kufanya maamuzi. Tunahitaji kuibadilisha miji yetu kuwa miji janja kwa kuwahamasisha watumiaji wa maji, na kubuni teknolojia itakayosimamia rasilimali maji inavyofaa.